0

Mambo 5 Ya Kuzingatia Kufanikisha Ndoto Zako 2021

Happy New Year #NdotoStar

Ni matumaini yangu kuwa mwaka mpya umeanza vyema kwako na kwa familia yako. Leo nina machache ambayo ningependa nikukumbushe uyazingatie ambayo nina amini yatakuwa na manufaa katika kutimiza ndoto zako mwaka huu. Kwa wale ambao wameshahudhuria vipindi vyangu Ndoto Hub wananijua mie mambo yangu huwa ni mafupi mafupi tu ???? Kwa wewe ambaye hatujakutana Ndoto Hub natarajia kukutana na wewe mwaka huu, ila kwa sasa chukua haya:
1. Jifahamu, Jikubali

Kwanza kabisa (kama bado hujafanya hivyo) jifanyie tathmini; ufahamu uwezo wako, mapungufu yako, fursa na changamoto zako. Tafuta mtu au watu wawili - watatu wa karibu yako, waombe wakufanyie tathmini. Usichukulie vibaya mrejesho wa tathmini za watu hao hasa pale unapoona wanakupa tathmini tofauti na unavyojitarajia au unavyojifahamu. Watu hao wanakuelezea namna wanavyopokea jinsi ulivyo, (Tuvute pumzi kidogo tulielewe hili: kuna namna ulivyo ambayo wewe unajiona, unajijua, alafu kuna namna ambavyo watu wanapokea jinsi ulivyo - haya mawili sio lazima yawe sawa wakati wote, ni matamanio yetu kuwa watu watupokee vile tunavyojiona sisi: ni kama vile ukiwa mwenyewe ukaimba unaweza kuamini kabisa huna tofauti kabisa na Vanessa Mdee, Zuchu au Beyonce ila ukijirekodi alafu ujisikilize ndio unaweza kuamua - basi tuchukulie tathmini zetu kutoka kwa watu wetu wa karibu kama kujisikiliza baada ya kujirekodi) chukua tathmini zote zitumie kama fursa ya kujifahamu na kujielewa zaidi. 


Pengine ni desturi au tamaduni zetu zimetujengea hali ya kuamini kuwa tunatakiwa kuwa wakamilifu kila wakati, ili hali tunajua hili haliwezekani; na inawezekana hali hii inatupeleka mahali ambapo hatujipi hata nafasi ya kujifahamu, kutambua na kukubali uwezo na mapungufu yetu. Kumbuka mapungufu sio kutokuwa kamili, uwezo wetu na mapungufu yetu ni sehemu ya sisi tulivyo, mapungufu yetu yanaweza kuwa ni fursa pia, hivyo ni bora ukayafahamu, yatambue alafu yakubali. Mpaka hapo utakuwa umeshapata majibu ni kwa namna gani basi unaweza kusonga mbele na kuwa wewe bora zaidi mwaka huu kutokana na uwezo na mapungufu uliyo nayo, mf. unaweza kujua ni mtu wa namna gani unamuhitaji kwenye biashara yako mwaka huu kama mbia, mshauri (mentor) au msaidizi n.k. Kutokana na kujijengea au kujengeka kwa hisia kuwa tunatakiwa kuwa wakamilifu, tunaweza kujikuta katika hali ambayo tunatumia nguvu nyingi na uwezo wetu mwingi kutaka kuyafunika yale tunayodhani ni mapungufu yetu, kiasi tunaweza kujikuta hatuweki kipaumbele kwenye uwezo wetu au yale mambo ambayo tunauwezo nayo sana. Basi, ufanye mwaka 2021 uwe mwaka wa kuyafanya yale ambayo una uwezo nayo, yafanye vizuri zaidi, jifunze vitu vipya vitakavyokusaidia kuuongezea uwezo wako. 


Bofya hapa kupata muongozo wa kufanya tathmini binafsi kwenye jukwaa la Ndoto Hub


2. Unaloweza Kulifanya Leo, Lifanye Leo

Umeamka mapema umeianza siku yako vizuri, umepanga mipango mingi ya kuboresha biashara yako; kujaribu vitu vipya kwenye bidhaa au huduma yako; unaanza shughuli zako ghafla simu au message inaingia, kuna dharura fulani, siku yako nzima inavurugika, Inakuwaje hii? Dada, binti, mama, mke, rafiki, mafanikio ya ratiba yako ya siku yanategemea vitu vingine vingi sana ambavyo viko nje ya uwezo wako nayo yaende sawa, mfano mtoto asiugue ghafla shuleni, au mzazi/mkwe asiwe na uhitaji na wewe ndani ya hiyo siku, n.k. hivyo ni bora tukajitahidi kila tunachopanga kufanya tukimalize ndani ya siku, tusijiwekee viporo mradi hatujui kesho itakuja na yapi. 


Angalizo: Hii isichukuliwe kumaanisha kuwa unatakiwa ufanye yote uliyopanga hata kama mwili au akili imeshachoka sana, fanya kwa kiasi kile ambacho una nguvu nacho ndani ya siku, lazima katika mpango wako wa siku kuwe kuna mpango wa muda wa kupumzika pia. Unapoamka na kupanga ratiba na mipango yako ya siku, zingatia pia uwezo wako na mapungufu yako (ile tathmini yako). Panga ratiba yenye uhalisia kwako na uhalisia wa maisha yako,  jipe nafasi na fursa ya kufanikiwa. Inawezekana siku yako au hata wiki yako huwa haiendi vile unavyopanga, angalia ni mambo ya aina gani huwa yanaingilia ratiba na mipango yako mara kwa mara. Kama ni mambo yale yale kuna mawili: inawezekana hayo ni mambo ambayo ni lazima uyazingatie na uyapange kwenye ratiba zako; au inawezekana ratiba unayoipanga wewe mwenyewe unaiogopa, hivyo kila mara unajipa nafasi au kujiaminisha kuwa hicho kingine kinachojitokeza ni cha muhimu zaidi kuliko mipango yako. Soma taratibu utanielewa... Sisi huwa tuna Ndoto kubwa sana, tuna mawazo, tuna mipango mikubwa sana kiasi sisi wenyewe tunaogopa hata kuanza kufanyia kazi, tunaogopa inaweza isifanikiwe, au pengine tunachoogopa haswa ni kuwa ndoto zetu zinaweza zikafanikiwa kiasi kikubwa sana zaidi ya matarajio yetu na hatuko tayari, kwa vyovyote vile, uoga huo ndio unaweza kupelekea sisi kutoweza kufuatisha ratiba zetu tunazojipangia wenyewe. 


3. Kuwa Mahali Pamoja kwa Wakati Mmoja 

Jinsi tulivyo na tunavyohitajika na watu wengi kunaweza kutupelekea kuwa watu ambao wakati wote tuko "kazini"; unaende kazini lakini uko busy "online" unapangilia shopping ya maharusi, mdogo wako anaoa/anaolewa; uko kwenye kikao cha VICOBA lakini unamalizia ya kaz?ni; uko kwenye kikao cha harusi una-chat na 'grupu' la VICOBA; uko harusini unapangilia kazi ya bosi, na kupanga ratiba ya chakula cha nyumbani kwa wiki inayofuata tena unatuma na message kwa "ma-supplier" wa sokoni wakuandalie vitu; na muda wa kufanyia kazi wazo lako la biashara unakuwa unachat na 'grupu' la familia/ukoo au la uliosoma nao. Pamoja na kwamba umekuwa "busy" sana kila mahali kila wakati, ukweli ni kwamba kote haupo.


Ufanye basi huu mwaka uwe mwaka wa kujifunza kuwa mahali pamoja kikamilifu, kama uko kwenye kujifunza ya biashara yako, jipangie muda wa kuingia shule, shule hiyo inaweza kuwa ni kuangalia YouTube, kusoma kitabu au "ku-Google" au kupitia account ya Instagram ya mtu/biashara inayofanya kitu unachokipenda wewe au kitakachokuwa na manufaa kwa biashara yako, jiwekee muda, mfano nusu saa au saa nzima ya kujifunza basi ingia kwenye hiyo shule kikamilifu. 


Lazima uwe na muda wa kutafuta masoko kwa undani na upana wake, hii ina maanisha pia kuwafahamu wateja na tabia zao (wateja ni wale wa sasa na wale ambao unataka wawe wateja wako); Uwe na muda wa kuelewa mambo ya fedha na vyanzo vyake kwa ajili ya biashara yako; Uwe na muda wa kufanya tafiti na majaribio ya kuboresha bidhaa au huduma zako pia; Jitengee muda wa kukaa na wafanyakazi au wasaidizi wako kwenye biashara, kuna mengi utajifunza kutoka kwao pia, utaweza kufahamu zaidi juu ya uwezo wao, ndoto zao na maoni yao ya jinsi ya kuboresha biashara, bidhaa au huduma yako, maana na wao ni watumiaji wako pia. 


Kama una mkutano wa VICOBA na mnaenda kujadiliana uwekezaji, basi jipe muda kwenye siku yako, fanya tafiti yako ndogo ya mambo ya uwekezaji kabla ya kikao, ukifika kwenye kikao uhudhurie kikamilifu na wewe uwe mchangiaji. Unapokuwa kwenye mambo ya kifamilia basi uwepo kikamilifu,  jipe muda wa kuwa na familia na watoto wako kikamilifu (bila simu au TV), jipangie ratiba, jipangie siku ya mapumziko na uutumie huo muda kupumzika.


4 Jipe Fursa ya Kujifunza Vitu Vipya 

Zaidi ya kujifunza mambo yote yanayohusiana na biashara yako na sekta nzima ya biashara yako, mwaka huu jipe fursa ya kujifunza kutoka kwa watu au vitu unavyoweza kuhisi havihusiani kabisa na wewe wala biashara yako. Mfano kama wewe uko kwenye sekta ya chakula, panga kuhudhuria mikutano au maonyesho ya mambo ya uziduaji (mining and extractives) au mambo yahusuyo mitindo, TEHAMA n.k. Jiunge kwenye vikundi, klabu au majukwaa ambayo katika hali ya kawaida usingefikiria kujiunga, mfano klabu ya wachoraji au anza kufanya kitu chochote ambacho kitakuwa ni kipya kwako. Hii itakupa fursa ya kupata mtazamo mpya juu ya biashara yako, au inaweza kukusaidia kuwaelewa vizuri zaidi watumiaji au wateja wako. 
Jipe fursa ya kutanua wigo wa mambo unayoyafahamu vizuri. Kujifunza na kufahamu mambo mapya kutakupa fursa au mwanya wa kupata mawazo mapya juu ya biashara, bidhaa au huduma yako. Hii iko ki-sayansi kabisa yaani ufahamu mpya au taarifa mpya ndio "charger" ya ubongo, jaribu leo. Pia ujuzi hauozi, zaidi ya kufahamu mambo mapya pia utakuwa umejiongezea "connection" na wadau wa biashara, bidhaa au huduma yako. 


5. Jifunze Kusamehe, Haraka, na Upesi

Mara nyingi tunapokuwa na wazo au ndoto fulani, huwa hatumshirikishi tu mtu yeyote, hii mara nyingi inatokana na ukubwa wa ndoto yetu. #NdotoStars wengi niliokutana nao husema wanaogopa kumshirikisha mtu kwa sababu wanahofia wazo litaibiwa, lakini nafikiri tukijitafiti na tukiwa wakweli na nafsi zetu tunaweza kukubali ukweli kwamba, unapokuwa na wazo lako au ndoto yako unatamani kila mtu aione ndoto yako au wazo lako kwa uzuri ule ule unaouona wewe. Pengine kutoshirikisha watu ndoto au mawazo yetu wakati mwingine kunaweza kuwa kunatokana na ukweli kwamba unaogopa asije akaliona wazo lako sio zuri kama wewe unavyoliona.


Tunapoamua kumshirikisha mtu mawazo au Ndoto zetu mara nyingi huwa tunafanya hivyo kwa mtu wa karibu sana, mzazi, dada/kaka, rafiki wa karibu, mwenzi wa ndoa n.k. Wakati unamshirikisha unakuwa katika hali fulani ya kujipanga, na pengine unapenda na yeye "ndugu msikilizaji" awe amekupa attention asilimia 100% ikiwezekana hata simu unaweza kumwambia aizime au aiweke silence kwa muda ili hali jambo unalotaka kumwambia ni kubwa, zito na la muhimu sana. Na huo ndio ukweli wa Ndoto zetu, ni mambo makubwa mazito ambayo yanaweza yakabadilisha kabisa maisha yetu, kwa uzuri au kwa ubaya.


Sisi ni viumbe tunaotegemeana, tunapomshirikisha mtu mwingine tunataka kupata uhakika wa mawazo yetu, na ndio maana maoni au mtazamo wa mtu wa karibu huwa yana uzito mkubwa, maneno anayosema baada ya kumshirikisha ndoto au mawazo yako, yanaweza kukujenga au kukuvunjavunja. 


Kama una mtu wa karibu ambaye kila unapomshirikisha jambo amekua akikupa moyo, akikuuliza maswali yenye kukufanya uboreshe mawazo yako na kusonga mbele zaidi, basi jihesabu ni mwenye bahati. Wengi wetu huwa tunakatishwa tamaa na watu wetu wa karibu, mwitikio wao unaweza kuwa "huwezi wewe" au {weka/igiza sauti ya mama wa kibongo} "mmmh utaweza wewe?" au "hakuna mtu kwenye familia/ukoo huu amewahi kufanya kitu kama hicho" na mengine mengi. Unaweza kuona ni maneno tu, lakini yana uzito sana kutokana na nafasi aliyopewa huyo mtu anayoyasema maneno hayo.


Inawezekana kabisa aliyekukatisha tamaa hakuwa na nia hiyo ila aliogopa kwa ajili yako. Mtu huyo anaona ukubwa wa ndoto yako na anakuhofia isipotimia, hivyo anajikuta anakutamania upunguze ukubwa wa ndoto yako. Umeshawahi kufikiria kuwa pengine anaona hivyo kutokana na ukweli kwamba huo ndio upeo wake? Hajawahi kuona mtu kama wewe, mwanamke kama wewe, mwenye umri kama wako, mwenye kila mazingira kama yako kufanikiwa kwa namna unayotamani wewe. Inawezekana pia katika upeo wake hajawahi kuona mwanaume anayem-support mke au mchumba wake au binti yake katika ndoto zake kwa kiasi hicho, hivyo mwitikio wake unaweza kuwa umetokana na wewe kumsukuma kwenye mambo asiyoyajua, ghafla.


Basi, leo tushushe pumzi, tuwasamehe wale wote waliotukatisha tamaa, msamehe kabisa. Kusamehe hakutayafuta wala hakutayarudisha yale maneno yake, bali kutayapunguzia makali na athari yake kwako. Unaweza kuchukulia mwitikio wake kama kiashiria kuwa una ndoto kubwa sana,  muombe aliyekukatisha tamaa akuelezee kwa mtazamo wake ni vitu gani anavyoona vitakufanya wewe ushindwe kufikia ndoto yako, hapa asikuambie "basi tu" (usizingatie kabisa mtazamo wa mtu anayekuambia "basi tu"), vitumie vitu hivyo kama fursa ya kuitazama upya ndoto yako katika mtazamo tofauti, (endapo ulikuwa hujavifikiria kabisa) basi angalia ni kwa jinsi gani unaweza kuvivuka vikwazo hivyo. 


Tujifunze kusamehe haraka haraka, tusibebe vitu mioyoni mwetu. Tayari una mzigo mkubwa sana wa kutimiza ndoto yako hatuhitaji mizigo mingine isiyo ya lazima. Zingatia kuwa kila anayekukwaza au kukukatisha tamaa ana upande wa pili aliotokea ambao pengine hauwezi kuujua lakini jua inawezekana kabisa hakuwa na nia mbaya kwako. Zaidi, jisamehe mwenyewe, jisamehe kwa kujiachia ukwazwe, jisamehe kwa kukosea, pia jisamehe kwani inawezekana na wewe umemkwaza mwingine kutokana na upeo wako. Jisamehe, samehe upesi upesi.

Nakutakia mwaka mpya wenye ndoto kubwa zaidi na mafanikio zaidi #AnzaNaNdoto

Iku.Kuhusu Ndoto Hub

Ndoto Hub ni jukwaa la wanawake wajasiriamali nchini Tanzania, lenye lengo la kuwakutanisha; kuwawezesha kufanikiwa kiuchumi kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uongozi (personal development & leadership); Ndoto Hub ni nafasi ya kufanyia kazi Ndoto zao;  pia ni jukwaa la taarifa na fursa za mitaji na masoko.  Ndoto Hub ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2018 ikiwa na tawi moja jijini Dar Es Salaam, tuko mbioni kufungua matawi zaidi ya Ndoto Hub katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania kuanzia mwaka huu 2021, STAY TUNED.


#NdotoStar ni mwanamke mjasiriamali mbunifu, mwenye umri kati ya miaka 19 hadi 30. Ni mwanadada mwenye ndoto kubwa ya ujasiriamali ambaye bado ana wazo au ambaye tayari ameshaanza kufanyia kazi ndoto yake. #NdotoStar ni dada jasiri, mwenye uthubutu, mwenye kujipa moyo kuwa anauwezo wa kuvuka vikwazo na mazingira yake kutimiza ndoto zake. Ni mdada ambaye yuko tayari kumsaidia na dada mwingine afanikiwe au afanikishe ndoto yake. #NdotoStar ni dada ambaye ndoto yake haimnufaishi yeye peke yake, bali jamii yote inayomzunguka. Je, wewe ni #NdotoStar na ungependa kujifunza na kushirikiana na #NdotoStars wengine? Karibu Ndoto Hub #AnzaNaNdoto


Iku ni mmoja wa wakufunzi wa Ndoto Hub, anafundisha #NdotoStars kujitambua, kujieleza na kueleza biashara zao (Personal Development & Communications)